UCHANGANUZI WA TASWIRA YA DINI KATIKA RIWAYA YA PARADISO: MTAZAMO WA KIDENGUZI
Loading...
Date
Authors
Journal Title
Journal ISSN
Volume Title
Publisher
THE CATHOLIC UNIVERSITY OF EASTERN AFRICA
DOI
Abstract
Dini ni mojawapo ya taasisi muhimu za kijamii zinazoathiri maadili, mitazamo, mahusiano na mienendo ya watu katika jamii mbalimbali. Katika fasihi ya Kiswahili, dini imekuwa ikisawiriwa kwa namna mbalimbali kutokana na nafasi yake katika maisha ya jamii, ikiwamo kujenga maadili, kutoa matumaini na kuathiri mahusiano pamoja na mamlaka. Hata hivyo, tafiti nyingi zilizotangulia katika fasihi ya Kiswahili zimejikita zaidi katika masuala ya kijamii na kisiasa, huku zikitoa nafasi finyu kwa uchanganuzi wa kina wa namna matini zinavyojenga, kuvuruga na kubadilisha maana ya dini na uongozi wa kidini. Pengo hili la kifasihi ndilo lililoongoza utafiti huu. Utafiti ulilenga kuchanganua taswira ya dini katika riwaya teule, kubainisha athari za dini katika maadili ya jamii katika riwaya teule, na kuchanganua usawiri wa viongozi wa dini katika riwaya teule. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Udenguzi iliyoasisiwa na Jacques Derrida na kuendelezwa na wanazuoni wengine, ambayo inasisitiza kuwa maana katika matini si thabiti bali inaweza kuvurugwa na kujengwa upya kulingana na muktadha. Mihimili mitatu ya nadharia hii ilitumika kuongoza uchanganuzi. Utafiti ulitumia muundo wa kimaelezo na ulilenga fasihi ya Kiswahili kama eneo la utafiti, huku riwaya ya Paradiso ikiteuliwa kimakusudi kama sampuli kwa sababu inabeba taswira pana na changamano za dini na viongozi wa dini. Data zilikusanywa kupitia usomaji wa kina wa riwaya teule zaidi ya mara moja, ambapo dondoo zinazohusiana na malengo ya utafiti zilitambuliwa, kunukuliwa na kuainishwa. Uchanganuzi wa data ulifanywa kimaelezo kwa kuhusisha dondoo za matini na mihimili ya Nadharia ya Udenguzi, huku ukizingatia mikinzano, maana zinazopingana na maana zilizofichika katika matini. Utafiti ulibaini kuwa taswira ya dini katika Paradiso ni pana na yenye sura zinazokinzana, ambapo dini inasawiriwa kama chanzo cha tumaini, wokovu na maendeleo, lakini wakati huo huo kama chombo cha migogoro, unyonyaji na ukandamizaji. Aidha, dini imebainika kuathiri maadili ya jamii kwa namna chanya na hasi. Kwa upande chanya, dini inahusishwa na kuimarisha umoja, uwajibikaji na mshikamano wa jamii, ilhali kwa upande hasi inahusishwa na chuki, unafiki, ubinafsi na migogoro. Viongozi wa dini wamesawiriwa kwa namna changamano, ambapo baadhi yao wanaonekana kuwa waaminifu na waadilifu, huku wengine wakidhihirisha udhaifu wa kibinadamu na matumizi mabaya ya mamlaka ya kidini. Kwa jumla, utafiti umebaini kuwa maana ya dini katika matini si thabiti, bali hubadilika kulingana na matendo ya wahusika, mazingira na muktadha wa matukio. Utafiti huu unapanua maarifa ya kifasihi kwa kuonyesha namna Nadharia ya Udenguzi inavyoweza kutumiwa katika uchanganuzi wa taswira ya dini katika riwaya ya Kiswahili. Inapendekezwa tafiti zaidi zichunguze taswira ya dini katika riwaya nyingine za Kiswahili, matumizi ya nadharia nyingine za uhakiki wa fasihi katika uchanganuzi wa dini, pamoja na usawiri wa viongozi wa dini katika kazi mbalimbali za fasihi.
Description
THESIS
